Description of PPIZ

Chuo cha kufundisha kilimo endelevu katika mazingira asilia kipo karibu na mji wa Zanzibar, katika kijiji cha Shakani Kisiwani Unguja. Chuo kinafunza kwa vitendo mbinu za ukulima endelevu bila ya kuathiri mazingira asilia ya eneo la uzalishaji. Tokea kuanzishwa kwake katika  mwaka 2016, chuo kimeweza  kuendeleza msitu ulionawiri wa mazao ya nchi za joto unaotoa taswira ya kile ambacho Chuo kimedhamiria kiendelezwe, yaani uwekaji wa hali kwa jamii kuishi katika mazingira muafaka kati yao na mazingira halisi.

Adhma ya Chuo ni kueneza ujuzi na taaluma endelevu ambapo itamwezesha binaadamu kuishi katika mazingira  bila  kutokea Athari kati ya mazingira na jamii na kuwa na hali ya usawa.

Kazi kuu ya Chuo ni kuwaelimisha wakulima wa kienyeji, wazalishaji  mboga mboga , wamiliki wa mashamba kuhusu  kilimo endelevu kwa lugha ya Kiswahili. Chuo huwa kinatoa mafunzo kwa vitendo kwa nusu siku juu ya utengenezaji mboji,/ utengenezaji wa udongo /dawa za kienyeji za kuzuwia wadudu waharibifu wa mimea/ upandaji wa mimea patanifu yaani mchanganyiko ya mimea inayoshirikiana katika  uzalishaji. 

Hata hivyo, chuo huwa kinatoa mafunzo ya msingi ambayo huwa yanaendeshwa kwa muda wa  kwa wiki mbili, ambayo yanajumuisha mada zifuatazo:

Misingi na maadili ya kilimo endelevu // Mpangilio wa Ramani na michoro  bora kwa uzalishaji endelevu katika eneo // Kupanga njia ya uvunaji wa maji ya mvua // Udhibiti na utumizi wa maji machafu yanayotokana na shughuli mbalimbali za ndani ya nyumba kama vile kupika, kufua au kukoga // Matumizi ya choo kisichotumia maji // Utengenezaji wa mboji kutokana na mabaki ya vitu mbalimbali kama chakula na majani // Utunzaji wa mbegu // Maangalizi wa vitalu kwa ajili ya mimea ya muda mrefu // Upangaji na utengenezaji wa  mitaro “swales” na mabwawa ya ufugaji // Ufugaji nyuki kitaalamu // Uzalishaji mazao mchanganyiko // Utengenezaji wa madawa ya kiasili kwa binaadamu // Uzalishaji wa miti ya misitu kwa kujiongezea kipato // Mifumo ya uzalishaji mifugo // Mafunzo katika maskuli kwa kuendeleza upatikanaji wa usalama wa chakula // Kuhuisha na kukuza nyungu nyungu kwa kuendeleza uzalishaji katika kilimo // Majiko bora yanayohitaji kuni chache // Ufugaji wa kuku na kuwatumia kwa kuchimbuachimbua na kuiongezea ardhi rutba

Mbali na mafunzo  ya kawaida ambayo yanakuwa yanatolewa na chuo kwa wote wale ambao  wanaongea    lugha ya Kiswahili, pia chuo kina endesha mipango miwili mikubwa ya masomo kama ifuatavyo: 

Program

FURSA KIJANI: huu ni mpango wa kuwajengea uwezo vijana ,ambapo vijana wa kizanzibari hupatiwa mafunzo   ya vitendo katka taasisi ya kilimo endelevu kwa muda wa wiki mbili ikifuatiwa na mafunzotarajali ya vitendo kwa miezi minne . Mafunzo hayo yanawawezesha vijana   kupata ajira ya utunzaji bustani na ukulima bora  na pia kuwawezesha kuanzisha shughuli za ujasiriamali mdogo mdogo katika shughuli za kilimo hai (ECOpreneurship).

BUSTANI ZA SKULI: huu ni mpango unaozihusisha skuli kutekeleza kilimo ndelevu kisichoharibu mazingira asilia mpango huu  unatekelezwa kwa ushirikiano na walimu, wanafunzi  pamoja na wanajamii karibu na skuli.  Chuo  kinasaidia kuandaa na kutekeleza mpango wa uzalishaji wa vyakula katika bustani za skuli, mafunzo ya nje ya darasa na kuhamasisha uhifadhi wa mazingira kupitia mitaala ya kawaida ya Skuli na kwa jamii kwa ujumla. Lengo  la mpango huu ni kuwashajihisha vijana tokea wakiwa na umri mdogo kupendelea kupanda mazao ya chakula , miti ya kutengenezea madawa na ile inayoleta haiba kutokana na kuvutia kwake na kufanya hali ya maisha kuwa bora zaidi. 

Shughuli nyengine zinazofanya na chuo hiki ni pamoja na:

Kutayarisha vitalu vya miti ya aina mbalimbali ikiwemo ya kabila za  kigeni na za kienyeji.

Kutengeneza mazao ya bustani ikiwemo mboji na madawa ya kienyeji kwa kukinga au kutibu maradhi mbalimbali ya mimea.

Kutoa huduma za ushauri wa utunzaji  wa bustani.

Kutayarisha na kutengeneza mwelekeo wa taswira nzuri ya bustani.

Kuandaa mafunzo kwa wafanyakazi au wanajamii juu ya miradi na shughuli tofauti.

Mafunzo ya kilimo endelevu “PDC” (kwa lugha ya Kiswahili} 

Huu mpangilio wa mafunzo uliotayarishwa kwa wakulima na watunza bustani ambao hukamilika kwa wiki mbili . Wahusika wanafunzwa kutunza bustani au kulima kulingana na mazingira halisi bila kuathiri mazingira ya eneo. Huduma zinazotolewa na chuo ni chakula na malazi. Pia huwepo safari za kimafunzo, na kualikwa wataalamu mbalimbali kushiriki kutoa mafunzo.  , hatimae  washiriki hutunukiwa vyeti baada ya  mafunzo hayo.